Monday, December 5, 2016

Upandaji na umwagiliaji pilipili mbuzi (habanero)






Maandalizi ya mbegu na kitalu cha pilipili mbuzi


Kila mara hakikisha unatumia mbegu bora. Bila kutumia mbegu bora huwezi kupata mavuno mazuri hata kama utafuata kanuni zote za kilimo bora chenye tija. Ni ukweli kwamba zao zuri linatokana na mche wenye afya nzuri. Ikiwezekana andaa miche yako katika trays na uiweke kwenye chumba maalum cha kukuzia miche (nursery) ili kuikinga na jua kali au mvua kubwa na wadudu washambulia miche.


 Kama unapanda katika kitalu hakikisha unautibu udongo kwa kuuchoma moto au kwa kutumia madawa mf Actara ili kuua mazalia ya wadudu yaliyopo katika udongo, udongo unatakiwa usiotuamisha maji na wenye rutuba ya kutosha. Pia kabla haujapanda mbegu hakikisha umezikinga na wadudu wanaobangua mbegu kuziweka dawa kama seed treat au seed care. Andaa tuta lenye urefu wa mita moja na upana wowote ambao utaweza kuumudu, chora vimistari kufuata upana wa tuta, kina kiwe inchi moja. Nafasi kati ya mstari na mstari iwe 10sm hadi 15sm. kisha upande mbegu zako kwa kufuata vimistari hivyo. Hakikisha mbegu hazijabanana sana ili kuzipa nafasi nzuri ya uotaji kisha fukia kwa udongo kiasi.

Maandalizi ya Shamba kwa ajili ya kilimo cha pilipili mbuzi (Habanero)


Ili kupata mazao bora inabidi kuandaa shamba vizuri kwa kulisafisha na kuondoa mabaki yote ya mazao ya zamani na kuyachoma moto ili kuondoa mazalia ya wadudu kutoka katika mazao yaliyopita.  Ni vyema kufanya kilimo cha mzunguko ili kuepuka wadudu kufanya makazi ya kudumu katika shamba lako. Kwa pilipili mbuzi ni vyema kuchagua shamba ambalo halijawahi kulimwa karibuni nyanya, tumbaku au viazi mviringo kwani wadudu wanaodhuru mazao haya wanadhuru pia pilipili mbuzi.

Maandalizi ya vifaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Hose Pipe 3"

Sucking pipe (koromeo)
Water pump BOSS WP80


Ili uweze kufanya kilimo chenye tija na cha kibiashara, ni lazima uchague zao ambalo litakupa faida nzuri zaidi kurudisha nguvu zako, muda wako na hata mtaji wako uliotumia. Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwenye kilimo kwa sababu mbali mbali ikiwemo:-
  •  Mtaji - Kama ilivyo katika biashara nyingine pia katika kilimo bila kuwa na mtaji wa kutosha huwezi kufanya kilimo cha kibiashara ni lazima ujue zao lako kabla ya kuanza kulima litahitaji mtaji wa kiasi gani. Vinginevyo unaweza kuishia njiani na hivyo kupata hasara kubwa.
  • Maarifa - Bila kuwa na maarifa sahihi juu ya zao unalotaka kulima ni rahisi kupata hasara. Ni lazima ujue ni mbegu gani nzuri, aina ya upandaji, maradhi, wadudu na muda wa kuweka mbolea na kipimo chake. 
  • Juhudi - Biashara hii ya kilimo hasa kilimo cha mboga mboga inahitaji usimamizi wa karibu. Ukiwa mzembe kwenye usimamizi ni rahisi kutokuvuna chochote au ukatumia gharama kubwa sana katika kukiendesha kutokana na wasamamizi utakaowaweka kutokuwa waaminifu. Ni vyema kabla hujaanza kulima kuhakikisha unao muda wa kuweza kusimamia shamba lako.
  • Masoko - Endapo usipokuwa makini katika masoko, mambo yote niliyoeleza hapo juu yanaweza yasiwe na maana hata kama uliyatekeleza kwa asilimia mia moja. Unaweza ukapata mazao bora na ya kisasa lakini yakaozea shambani kwa kukosa soko na hivyo kupoteza mtaji na nguvu zako. Kabla hujaanza kulima lazima ujue soko la zao utakalolima pindi uvunapo. Ni lazima ufanye utafiti wa soko kwa kupata majibu ya maswali yafuatayo: Je ni wakati gani zao fulani linaadimika sokoni? Je hilo zao wateja wanapenda la aina gani, kama ni nyanya je wanapenda kubwa au ndogo ndogo au za wastani?  Je gharama za uzalishaji ni ndogo kuliko faida kwa makadirio ya chini nayotegemea kupata? Ukipata majibu ya maswali hayo ndio uingie kuanza kulima huku ukijua muda utakaovuna mazao yako bei ya soko inatazamiwa kuwaje.